MILIO ya risasi na milipuko mikubwa ya mabomu imesikika karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa nchini Niger, na kusababisha taharuki.
Video ziliozosambaa mitandaoni mapema leo Januari 29, 2025 zilionyesha mifumo ya ulinzi wa anga katika mji mkuu wa Niamey, ikishambulia makombora yasiyotambulika yanatoka wapi.
Hata hivyo, hali ilitulia baadae, huku ofisa mmoja akiripotiwa kusema hali ilikuwa imedhibitiwa, bila kufafanua zaidi.
Haijulikani ni nini kilisababisha milipuko hiyo, au kama kulikuwa na majeruhi katika tukio hilo.
Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na serikali ya kijeshi kuhusu mkasa huo.
Shirika la habari la AFP, liliripoti kuwa milio ya risasi na makombora ilianza kusikika muda mfupi baada ya saa sita usiku.
Kwa mujibu wa wakazi wanaoishi katika kitongoji kilicho karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani, hali ya utulivu ulirejea baada ya saa mbili.
Uwanja wa ndege una kituo cha jeshi la anga na uko takriban kilomita 10 (maili sita) kutoka ikulu ya rais.
Niger inaongozwa na Abdourahamane Tiani ambaye alichukua madaraka katika mapinduzi ya 2023.
Kama majirani zake Burkina Faso na Mali, nchi hiyo imekuwa ikipambana na makundi ya jihadi ambayo yamefanya mashambulizi ndani ya eneo hilo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED