slot gacor
slot gacor
slot gacor
Museveni aomba pingamizi dhidi ya ushindi wake litupiliwe | Nipashe

Museveni aomba pingamizi dhidi ya ushindi wake litupiliwe

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:26 PM Jan 28 2026
Rais mteule wa Uganda, Yoweri Museveni.
Picha:Mtandao
Rais mteule wa Uganda, Yoweri Museveni.

Rais mteule wa Uganda, Yoweri Museveni, amewasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Uganda akiitaka itupilie mbali pingamizi lililowekwa dhidi ya ushindi wake wa urais, akisisitiza kuwa uchaguzi wa Januari 15 ulifanyika kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Kupitia wakili wake, Museveni ameeleza kuwa licha ya kuwepo kwa madai ya dosari ndogo, ambazo amezikanusha vikali, makosa hayo hayakuwa na uzito wa kuathiri matokeo ya uchaguzi wala kuhalalisha kufutwa kwa uchaguzi wa urais. Amesema mchakato mzima wa uchaguzi ulifuata misingi ya kisheria na taratibu zilizowekwa.

“Nilichaguliwa kwa mujibu wa kanuni zilizobainishwa katika Katiba, Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi wa Rais,” Museveni alinukuliwa akieleza mbele ya Mahakama Kuu.

Pingamizi hilo lililowasilishwa Januari 17 na Bwana Kasibante linadai kuwa mchakato mzima wa uchaguzi nchini Uganda, kuanzia usajili wa wapiga kura, upigaji kura, hadi kuhesabu na kutangaza matokeo, ulikumbwa na ukiukwaji mkubwa wa Katiba, Sheria ya Tume ya Uchaguzi pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Rais.

Kasibante pia amemshutumu Museveni kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya serikali katika kuchochea vurugu, vitisho na kuvuruga mikutano ya wagombea wa upinzani pamoja na wafuasi wao. Hata hivyo, Museveni amekanusha vikali madai hayo kupitia hati yake ya utetezi iliyowasilishwa jana, Siku ya Ukombozi ya chama cha NRM.

“Mshitakiwa wa kwanza, Museveni, anakataa kabisa madai kuwa alitumia vikosi vya ulinzi kuendeleza vurugu dhidi ya wagombea wa upinzani au kwa namna yoyote ile. Hakukuwa na vurugu zilizofanywa kwa uelewa, ridhaa au idhini yake,” ilieleza sehemu ya utetezi huo.

Aidha, Museveni ametetea uhalali wa mchakato wa kuhesabu, kujumlisha na kuwasilisha matokeo ya uchaguzi, akisisitiza kuwa ulifanyika kwa uwazi na uwajibikaji, mbele ya wagombea na mawakala wao.

Mahakama Kuu ya Uganda, chini ya Jaji Mkuu Flavian Zeija, inatarajiwa kutoa maelekezo na maamuzi ya kisheria ili kuhakikisha pingamizi hilo linakamilika ndani ya siku 30 kama inavyotakiwa na sheria.

Hatua hii inajiri wakati ambapo mpinzani mkuu wa Museveni, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, alitangaza kuwa hana nia ya kufungua shauri mahakamani, akidai uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki.