Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, amefanya ukaguzi wa mradi wa uchimbaji wa kisima kirefu katika eneo la chanzo cha maji Sinde, Manispaa ya Lindi, mradi unaolenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Ukaguzi wa mradi huo ulifanyika jana unatekelezwa na wataalamu wa ndani kwa uwezeshaji wa Ofisi ya Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lindi, kwa kushirikiana na Chombo cha Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii cha Kuchele (CBWSO). Utekelezaji wa kisima hicho umekamilika, kikiwa na ukubwa wa inchi nane na kugharimu jumla ya shilingi milioni 39.
Akitoa taarifa ya mradi, Mhandisi William Swila amesema kisima hicho kina urefu wa mita 175 na kinatarajiwa kutoa maji takribani lita 60,000 kwa saa moja, huku kikihudumia wananchi wasiopungua 25,000. Alieleza kuwa kazi zilizotekelezwa ni pamoja na utafiti wa maji ardhini, uchimbaji wa kisima, usafishaji wa kisima pamoja na kazi nyingine zote za kitaalamu zinazohusiana na ujenzi wa mradi huo.
Mhandisi Swila aliongeza kuwa mradi huo utaondoa changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kata tano za Halmashauri ya Mtama. Amesisitiza kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutekeleza azma ya “kumtua mama ndoo kichwani”.
Kwa upande wake, Mwanziva alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya kusambaza magari ya kuchimba visima nchi nzima, hali iliyoifanya Mkoa wa Lindi kunufaika moja kwa moja na huduma hiyo. Aidha, ametoa pongezi kwa Wizara ya Maji, RUWASA, CBWSO pamoja na wataalamu wote walioshiriki katika utekelezaji wa mradi huo.
Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo yanayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi, hususan katika sekta muhimu kama maji. Amehitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kuitunza na kulinda miundombinu ya maji ili kuhakikisha inakuwa endelevu na kuendelea kutoa huduma bora, safi na salama kwa muda mrefu.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED