Mbunge wa Mwibara Kangi Lugola, amesema kundi la ‘Machawa’ kama halitadhibitiwa litachangia kuharibu mipango ya serikali kudhibiti ufisadi pamoja na ubadhirifu nchini.
Lugola, amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma, wakati akichangia mjadala wa hotuba ya Rais aliyoitoa Novemba 14, 2025 alipolizindua rasmi Bunge la 13.
“Mheshimiwa
mwenyekiti machawa ni kundi hatari ndimo wanamojificha mafisadi, ndimo wanamojificha wabadhirifu na bila kushughulika na machawa ambacho ni kichaka wanamojificha kukichoma moto na kukifyekerea mbali maono yote ya serikali yatafanikiwa,”amesema
Amesema lazima pia serikali ingalie mambo kadhaa, ikiwamo kuhakikisha kuwa mihimili ya dola, mahakama, bunge pamoja na serikali inakuwa ni huru.
“Bunge liwe huru, leo tukiletewa taarifa ya CAG, mfano lazima tuijadili kwa uhuru kwa upana ili tushughulike na wabadhirifu, ndipo maono ya mheshimiwa Rais yatakapofikiwa, tutakapo weka maazimio lazima yaende yaheshimiwe na serikali na serikali iyatekeleze bila hivyo hatutafanikiwa,”amesema.
Pia mahakama inapaswa kuwa huru wakipelekewa watu ambao wamefanya uhalifu watendewe haki ya kuhukumiwa ili waogope fedha za serikali.
“Vyombo vya kiuchunguzi na vyenyewe lazima viwe huru lazima mwendesha mashtaka awe huru ili maono hayo yafikiwe, lazima polisi wawe huru ili wachunguze watu ambao mafisadi papa wapelekwe mahakamani kuliko kupeleka vidagaa, vimjusi vidogovidogo ndivyo vinakwenda mahakamani,”amesema Lugola .
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED