Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, limeazimia kufuta mfumo wa kupitisha kampuni moja kununua zao la pamba kutoka kwa wakulima, badala yake limeruhusu makampuni mbalimbali kushiriki katika ununuzi huo.
Uamuzi huo umetolewa jana katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani cha kupokea na kujadili taarifa ya maendeleo ya halmashauri kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Joseph Limbe amesema madiwani wameazima kufuta mfumo huo kutokana na malalamiko ya muda mrefu ya wakulima kuhusu pamba yao kununuliwa kwa bei ndogo.
Amesema, mfumo huo wa kampuni moja umekuwa ukimkandamiza mkulima kiuchumi ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo wakulima waliuza pamba yao kwa makampuni mbalimbali hivyo kunufaika kutokana na ushindani wa bei.
“Baraza limeazimia kuufuta mfumo wa mnunuzi mmoja wa zao la pamba, na badala yake kuruhusu makampuni mbalimbali kununua, ili kuwepo na soko huria lenye ushindani wa bei hivyo kumuinua mkulima kiuchumi,” amesema Limbe.
Ameongeza kuwa, uamuzi huo unaakisi dhamira ya dhati ya madiwani katika kusimamia maslahi ya wakulima, pamoja na kukuza kilimo cha pamba kama zao muhimu la kiuchumi katika wilaya hiyo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED