Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanya ukaguzi wa kitaalamu wa mita za umeme kwa baadhi ya wateja waliowasilisha malalamiko hayo kwa njia za mitandao katika maeneo ya Tabata Kimanga na Kimara Suka jijini Dar es Salaam.
Malalamiko hayo yaliibuliwa na baadhi ya wananchi mitandaoni na kwenye vyombo vya habari kuhusu madai ya umeme kuisha haraka bila sababu ya msingi.
Zoezi hilo lilifanyika Januari 27, 2026, likiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowelle, akiambatana na timu ya wataalamu wa Shirika, kwa lengo la kubaini chanzo halisi cha changamoto hiyo na kujiridhisha kuhusu ufanisi wa utendaji wa mita za wateja.
Matokeo ya Ukaguzi
Baada ya kufanyiwa vipimo vya kitaalamu, TANESCO imebaini kuwa mita zote zilizokaguliwa zilikuwa salama na zinafanya kazi kwa usahihi, kinyume na madai yaliyokuwa yakitolewa kuwa mita hizo zina kasoro ya kiutendaji.
Hata hivyo, ukaguzi umeonesha kuwa vyanzo vilivyopelekea wateja waliokaguliwa kulalamika umeme kuisha kwa haraka ni uchakavu wa mtandao wa nyaya za umeme (wiring) ndani ya nyumba, hali iliyosababisha umeme kuvuja bila mtumiaji kugundua.
Aidha, matumizi holela ya umeme yameonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Gowelle amesema
“Baada ya kuona malalamiko yanaongezeka, tuliona ni muhimu kufika moja kwa moja kwa baadhi ya wateja waliolalamika. Tulifanya ukaguzi wa kitaalamu, tukazima vifaa vya umeme na kufuatilia usomaji wa mita, lakini bado uniti ziliendelea kupungua. Hii ilithibitisha kuwepo kwa hitilafu katika mfumo wa wiring za ndani ya nyumba na sio mita."
Katika nyumba moja iliyopo Tabata, ukaguzi ulibaini kuwa uchakavu wa mtandao wa nyaya (wiring) ulisababisha upotevu wa takribani uniti mbili za umeme, hali iliyomfanya mteja kutumia zaidi ya shilingi 30,000 za ziada kwa mwezi kuliko matumizi yake halisi.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED