TUME ya Ulinzi wa Taarifa (PDPC), imesema kuwa unapokwenda nyumba ya kulala wageni hairuhusiwi kuandika ulikotoka na unakokwenda kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria ya taarifa binafsi.
Akiwasilisha mada ya zana ya taarifa binafsi, Mkurugenzi wa usajili na Uzingatiaji wa PDPC, Stephen Wangwe, amesema ni muhimu watu wakaijua sheria ili kuepuka kuingia kwenye matatizo, na kwamba kwa kuandika mtu anatoka na kwenda wapi au kabila lake havihusiani na yeye kufikia kwenye nyumba aliyokwenda kulala.
“Unakwenda nyumba ya kulala wageni unaambiwa andika ulikotoka na unakokwenda, kabila lako lakini haya yote ni taarifa binafsi na wanavunja sheria. Au kipindi cha nyuma matokeo ya mitihani yalikuwa yanatangazwa kwa majina, inatakiwa kuweka namba ili kulinda taarifa za mtu,”amesema.
Amesema tangu kuwepo kwa sheria hiyo mtu anapoona taarifa zake zimetumika bila ridhaa yake anaruhusiwa kulalamika kisha hatua zitafuatwa dhidi yake.
“Taarifa zako zikitumika vibaya na huna kokote pa kulalamika maana yake hutakuwa na imani na huduma husika, kutokana na hali hiyo wapo ambao hawatoi fedha kwenye ATM hadi aende ndani ya benki, na kwamba baadhi ni kwasababu wameshaumizwa kwa taarifa zao binafsi kuwa hadharani,”amesema.
Wangwe amesema sheria imekuwepo ili kurudisha imani kwa watu, wote wanaochakata taarifa binafsi wanasajiliwa, kusikilzia, usuluhishi hadi mtu atakapopata haki yake.
Aidha,amesema misingi ulinzi wa taarifa binafsi ni mkusanyaji au mchakataji akusanye kihalali, afanye kwa haki bila kuonea, afanye kwa uwazi anakusanya kwa ajili gani na lengo gani na madhumuni mahususi asivuke mpaka wake.
Mingine ni kukusanya kwa utoshelevu na asikusanye chini ya kiwango au zaidi ya kiwango kinachohitajika; taarifa zitoke kwa muhusika na zisionekane kwa wasiohusika, lazima ziwe sahihi na ziende na wakati; kuhifadhi taarifa hairuhusiwi kuhifadhi chini ya muda au zaidi ya muda husika.
Misingi mingine ni taarifa zinazovuka nje ya mipaka ya nchi na kwamba kwasasa ukitaka kupeleka taarifa nje ya nchi ni lazima kupata kibali cha nchi ili kujua zinakwenda wapi, kuna ulinzi wa kutosha wa taarifa zake na kwamba kuna fomu namba saba ya kujaza na kikubwa kuhakikisha zinapotoka ziwe na uhakika wake.
Amesema kuna mifumo 850 imeunganishwa na NIDA na kwamba kabla ya kuunganishwa na lazima apate cheti cha idhini kabla ya kuzitumia, “Kokote ambako taarifa yako itatumiwa na mtoa huduma yeyote utapata ujumbe ili uwe na ridhaa kwenye taarifa zako.”
Amesema faida ya Sheria ya Taarifa Binafsi itaongeza ubunifu, kumlinda mwenye taarifa, inampa nguvu na kuhakikisha mambo yanakuwa wazi, inaongeza ushindani, inalinda faragha, ukiona taarifa zako zimesambazwa bila ridhaa yako una haki ya kulalamika.
Wangwe amesema pia ni kuhakikisha inajulikana taarifa za unatoka wapi unakwenda wapi haziwahusu wanakusanya taarifa za ziada ambazo sio zao, pia wanaotoa matokeo hawaruhusiwi kutangaza majina bali kuweka namba pekee.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED