slot gacor
slot gacor
slot gacor
Masauni: Samia aongoza mapinduzi uhifadhi mazingira | Nipashe

Masauni: Samia aongoza mapinduzi uhifadhi mazingira

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:32 PM Jan 27 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amesema uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, umeiwezesha nchi kupiga hatua kubwa katika uhifadhi wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha Muungano kwa kuzingatia misingi ya maendeleo endelevu.

Masauni ameyasema hayo Januari 27, 2026 katika hafla ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya Rais Dk. Samia  iliyofanyika Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo Rais aliongoza zoezi la kupanda miti kama sehemu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Amesema chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kimkakati katika sekta ya mazingira, ikiwemo kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.

Ameeleza kuwa Rais Samia pia ameongoza juhudi za kimataifa za kutafuta rasilimali za kifedha kwa ajili ya nishati safi ya kupikia barani Afrika, hatua iliyoongeza fursa kwa Tanzania kunufaika na mifumo ya ufadhili wa kimataifa katika masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Hatua hizo zimechangia Rais kutambuliwa kitaifa na kimataifa kama kiongozi anayelipa kipaumbele suala la mazingira.

“Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, Tanzania imeanzisha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Biashara ya Kaboni, hatua inayoiwezesha nchi kunufaika zaidi na fursa za soko la kaboni sambamba na kuongeza mapato yatokanayo na uhifadhi wa mazingira,” amesema Mhe. Masauni.

Ameongeza kuwa fedha za mazingira na mabadiliko ya tabianchi zimeongezeka kupitia vyanzo vya ndani na nje, sambamba na kuanzishwa kwa Kitengo Maalum cha Fedha za Mabadiliko ya Tabianchi. Aidha, kwa mara ya kwanza Tanzania imepata Dira ya Taifa ya Maendeleo inayotambua mazingira na uhimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kama nguzo mahsusi ya maendeleo, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2025–2030) yenye vipaumbele vya uhifadhi wa mazingira.

Kuhusu Muungano, Masauni amesema Rais Samia amewezesha kutatuliwa zaidi ya hoja 15 kati ya hoja 18 za Muungano alizozikuta, jambo lililoimarisha mshikamano, amani na utulivu kati ya pande mbili za Muungano.

Vilevile, amesema Rais ameiongoza nchi kuandaa Sera ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 inayolenga kuimarisha sekta za uchumi wa buluu kwa misingi ya uendelevu ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

Masauni amewahamasisha Watanzania kuiga mfano wa Rais Samia kwa kuadhimisha matukio muhimu ya maisha yao kwa kupanda miti na kuitunza hadi ikue. Amesema endapo Watanzania milioni 30 wangepanda mti mmoja kila mmoja katika siku zao za kuzaliwa, taifa lingeongeza angalau miti milioni 30 kila mwaka, hatua itakayosaidia kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.