Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Chacha Wambura, amehoji Bungeni hatua zilizofikiwa na Serikali katika kuendeleza na kukamilisha ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Manispaa ya Geita ulioanza kujengwa mwaka 2021.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya afya, Rajabu Seif, amesema ujenzi wa uwanja huo ulianza mwaka 2021 kwa kutumia fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) kwa gharama ya Sh bilioni 5.46.
Amesema ujenzi ulisimama mwaka 2023 ukiwa umefikia asilimia 71 baada ya mkandarasi kusitishiwa mkataba kufuatia mabadiliko ya kanuni za CSR. Seif amesema Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Geita Gold Mining (GGM) imepata mkandarasi mshauri anayefanya mapitio ya gharama halisi za kukamilisha ujenzi huo, ambapo kiasi cha takribani Sh bilioni 5 kinahitajika ili kuukamilisha.
Ameongeza kuwa Serikali kwa sasa inapitia gharama zilizowasilishwa na mkandarasi mshauri kwa lengo la kuendelea na ujenzi kwa kutumia fedha za CSR katika mwaka wa fedha 2026/2027. Katika swali la nyongeza, Mbunge Wambura alihoji kwa nini mapitio hayo yasifanywe kwa haraka ili uwanja ukamilike mapema na kutumika kwenye maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), akieleza kuwa Geita ipo katikati ya nchi za Kenya na Uganda na inaweza kutumika kama kituo cha mazoezi kwa timu zitakazoshiriki mashindano hayo.
Pia amehoji kama Serikali haioni haja ya kushirikiana zaidi na sekta binafsi katika ujenzi wa viwanja na kuendeleza michezo nchini.Akijibu, Naibu Waziri Seif alisema Sh bilioni 3.4 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha jukwaa kuu, majukwaa ya watazamaji na eneo la kuchezea mpira, na kwamba kazi hizo zinatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2026. Amesema Serikali inatambua umuhimu wa uwanja huo kwa maendeleo ya michezo na burudani, akibainisha kuwa Mkoa wa Geita una zaidi ya watu milioni tatu.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED