Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe limekanusha vikali taarifa zilizokuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii nchini, zikiambatana na picha mjongeo (video), zilizodai kuwa kuna Askari Polisi wa mkoa huo aliyekuwa amechomwa moto na kuporwa silaha.
Akizungumza Januari 28, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mahamoud Banga, amesema kuwa katika Mkoa wa Njombe hakuna tukio lolote la aina hiyo lililotokea, akionya dhidi ya watu wanaoandaa na kusambaza taarifa za uongo na za kupotosha umma.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wachache wenye tabia ya kuandaa na kusambaza taarifa za uongo na upotoshaji kwa njia mbalimbali kuacha mara moja, kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria za nchi na maadili ya Mtanzania. Aidha, hakuna faida yoyote kwa wanaofanya vitendo hivyo, familia zao wala jamii kwa ujumla,” amesema ACP Banga.
Kamanda Banga ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwafuatilia mtu au watu waliochukua na kutumia picha mjongeo ya tukio la zamani, ambapo askari walikwenda kutoa msaada kwa wananchi, na kisha kuibadilisha na kuisambaza kama taarifa ya uongo kupitia mitandao ya kijamii.
Aidha, amesema Polisi Mkoa wa Njombe wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa kushirikiana na wananchi kupitia programu za Polisi Jamii, kwa lengo la kubaini na kuzuia uhalifu. Hatua hizo zinaenda sambamba na kuimarisha doria, misako na operesheni mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa maisha na mali za wananchi unalindwa wakati wote.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED