Taasisi za umma na binafsi 9,000 nchini zimejisajili kwenye Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki.
Waziri huyo alitoa agizo na kuongeza muda wa miezi mitatu kuanzia Januari 8 hadi April 8, 2026 ili kuhakikisha taasisi zote, zinakamilisha kwa hiari usajili wa taarifa katika kipindi hicho. Mkurugenzi wa PDPC Dk. Emmanuel Mkilia ameyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Faragha duniani, ambayo uadhimishwa Januari 28 ya kila mwaka.
Dk. Mkilia amesema kuwa hatua hiyo inaonyesha tayari kuna mwamko wa taasisi na wananchi kuhusu ulinzi wa taarifa zao binafsi baada ya tume hiyo kutoa elimu na kuhakikisha taasisi zinazosajiliwa ni zile zinazohusika na kukusanya, kuhifadhi, kuchakata na kusafirisha taarifa nje ya nchi.
“Sheria inamlinda raia ambaye mara nyingi ndiye mtumiaji wa mwisho wa teknolojia, lakini katika baadhi ya nyakati taarifa zake zinageuzwa kuwa kama bidhaa, hivyo ni muhimu kuelewa haki zake, msingi wa ulinzi wa taarifa binafsi unaanza kutoka kwake,”anasema. Ameongeza pia wanaokusanya na kuchakata taarifa, wanapaswa kuhakikisha wanatambua wajibu wao wa kulinda taarifa binafsi wanapotekeleza majukumu yao.
Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji wa PDPC, Mhandisi Stephen Wangwe,alisema kuwa taarifa binafsi ni zile zinazomtambulisha mwananchi, mfano taarifa za afya, kabila, kazi, hali ya maisha, au mawasiliano yake. Ameongeza kuwa kuna taarifa za faragha ambazo mtu anaweza kuamua ni kiasi gani angetaka watu wengine wajue, na jinsi anavyotaka zijulikane.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED