slot gacor
slot gacor
slot gacor
TAMISEMI yasisitiza elimu stadi maisha | Nipashe

TAMISEMI yasisitiza elimu stadi maisha

By Christina Haule , Nipashe
Published at 11:48 AM Jan 27 2026
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Riziki Shemdoe, amewasisitiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Idara na Taasisi nchini kuipokea na kuhakikisha elimu ya stadi za maisha inatekelezwa ipasavyo, ili kuwasaidia wanafunzi, hususan wa kike, kupata manufaa ya kielimu.

Shemdoe ameyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka 2025 wa CAMFED unaofanyika mkoani humo, ukiwa na kauli mbiu “Wekeza Elimu kwa Maendeleo Endelevu.” Amesema mradi huo unatekelezwa na Kampeni ya Kusaidia Wasichana Nchini (CAMFED).

Ameeleza kuwa licha ya mradi huo kutekelezwa katika mikoa 10 pekee kwa ushirikiano wa CAMFED na Serikali na tayari kuonesha manufaa, mikoa yote inapaswa kusimamia utekelezaji wake ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa CAMFED, Anna Sawaki, amesema jumla ya shilingi bilioni 28 zimetumika kuwawezesha wanafunzi kielimu. Amesema kwa mwaka 2025 pekee, wanafunzi 38,928 wa shule za sekondari na wanafunzi 1,277 wa vyuo na vyuo vikuu wamenufaika kwa kulipiwa ada, kupatiwa vifaa vya shule na chakula.

Sawaki amesema fedha hizo zimetokana na michango ya wafadhili pamoja na Serikali, huku akibainisha kuwa lengo la CAMFED ni kuhakikisha asilimia 85 ya shule, mikoa na halmashauri zinawezeshwa katika sekta ya elimu ifikapo mwaka 2029/30.

Ameongeza kuwa CAMFED imejipanga pia kuwafikia vijana 9,027 kwa kuwawezesha kiuchumi kupitia elimu ya ujasiriamali na mikopo.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Yasinta Nzogela, ameishauri CAMFED kushirikiana na Serikali kuandaa mwongozo wa mtaala wa amali utakaoinua vijana katika masomo ya kilimo na kuondoa dhana potofu inayowafanya wanafunzi kuliona kilimo kama adhabu badala ya fursa na mtaji.

Mmoja wa wanafunzi walionufaika na mradi wa CAMA, Habe Tambala kutoka Shule ya Sekondari Mikese, ameishukuru CAMFED kwa kumuwezesha kuendelea na masomo kwa kumpatia vifaa vya shule na chakula, hali iliyomrejeshea ndoto yake ya kuwa daktari iliyokuwa imezimika baada ya ndugu aliyekuwa akimsaidia kuhama mkoa.