Watuhumiwa wawili, Amasha Iddi Mrisho (40), mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam, na Seleman Juma Ally (32), raia wa Msumbiji, Januari 22, 2026, wamefikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke kujibu tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya skanka.
Akisoma maelezo ya awali ya shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi, Lukosi, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Wakili Nicas Kihembe, akisaidiana na Erick, alidai kuwa washtakiwa hao walikamatwa Desemba 08, 2025, katika Mtaa wa Wailes, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, na maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Ilidaiwa mahakamani kuwa, katika operesheni hiyo, maofisa wa DCEA walikamata pakiti 20 za bangi aina ya skanka zenye uzito wa jumla wa kilogramu 20.03. Dawa hizo zilielezwa kuwa zilifichwa ndani ya balo la nguo za mitumba na kusafirishwa kwa kutumia basi aina ya Scania la kampuni ya King Masai Tours, lenye namba za usajili AAM 297 CA, likitokea Msumbiji.
Upande wa mashtaka ulieleza kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kosa la jinai chini ya kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, kinachokataza umiliki, usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya nchini.
Mwendesha mashtaka aliiambia mahakama kuwa shtaka hilo halina dhamana kutokana na uzito wa dawa za kulevya walizokutwa nazo washtakiwa.
Aidha, mahakama ilielezwa kuwa upelelezi wa shauri hilo namba 1535/2026 bado unaendelea, huku mashahidi wakitarajiwa kufikishwa mahakamani siku itakayopangwa.
Mahakama imeahirisha shauri hilo hadi Februari 05, 2026, na kuamuru washtakiwa warejeshwe rumande.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED