Watu wawili ambao hawajafahamika majina yao wameuawa kwa kuchomwa moto huku gari aina ya fuso nalo likiteketezwa kwa moto na wananchi wa Kijiji cha Isalalo, Wilayani Mbozi, baada ya kutuhumiwa kuiba ng’ombe nane.
Pia, katika tukio hilo lililotokea Januari 28,mwaka huu inadaiwa ng’ombe hao walitoroshwa na watu wasiojulikana mara baada ya wezi hao kudhibitiwa na hatimaye kuuawa kwa kuchomwa moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa jeshi hilo linamshikilia dereva wa gari aina ya Fuso lenye namba T 934 BQ, mali ya Aseneje Mkumbwa, lililotumika kubeba ng’ombe hao, Kennedy Mwaluvanda, mkazi wa Nanenane, jijini Mbeya, kwa mahojiano zaidi.
Amesema watu hao wanadaiwa kuiba ng’ombe hao katika Kijiji cha Tindingoma, Wilayani Momba. “Watu hao waliuwawa baada ya wananchi kupewa taarifa ya wizi wa ng’ombe kutoka kwa wenzao wa Wilaya ya Momba, ambapo walijikusanya, kuweka doria, na kufanikisha kuwakamata wawili hao na kuwachoma moto, pamoja na gari lililotumiwa kubeba ng’ombe hao,” amesema Kamanda Senga.
Polisi wanaendelea na msako wa watu wengine wawili wanaodaiwa kuhusika kwenye wizi huo, lakini walifanikiwa kutoroka.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED