MIKEL Arteta, amefichua kwamba aliwaita wachezaji wake kwa ajili ya mkutano “wa kupunguza joto” na akawasihi mashabiki wa Arsenal kutokuwa na hofu baada ya kufungwa na Manchester United.
Mwelekeo wa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa Arsenal ulipata pigo baada ya kuchapwa 3-2 na Man United katika Uwanja wa Emirates Jumapili.
Kikosi cha Arteta kimechukua pointi mbili tu kati ya tisa katika mechi zao tatu zilizopita.
Hata hivyo, Arsenal inaongoza msimamo kwa tofauti ya pointi nne mbele ya Manchester City inayoshika nafasi ya pili, pia wapo njiani kufikia fainali ya Kombe la Carabao na wapo pia kwenye Kombe la FA.
Arteta aliiambia Sky Sport: "Mwitikio wa wachezaji tangu kufungwa na Man United umekuwa bora. Tulichukua muda wa kupunguza joto, kusimama, kutafakari na kuulizana maswali.
"Moja lilikuwa: 'Tunahisi vipi? Na mimi mwenyewe ninajisikiaje?' Na kisha: 'Tunataka kuishi vipi miezi minne ijayo?'
"Yalikuwa mazungumzo ya kutia moyo na mazuri sana, kwa sababu wote tunajua tunachokitaka.
"Tumepata haki ya kuwa katika nafasi nzuri kwenye mashindano manne, na katika miezi minne ijayo tutaishi na kucheza kwa furaha, kwa ujasiri mwingi na kwa imani kwamba tutashinda.
"Hii nzuri kwetu na tutaweka nguvu zetu, na ninatumaini tu kwamba kila mtu anayehusiana na klabu hii, haswa mashabiki wetu, watakuwa na imani."
Aliongeza: "Tunafanya hivyo kila baada ya wiki tatu hadi nne. Ni muhimu sana kuelewa ukweli dhidi ya mtazamo, na wakati mwingine inabidi uangalie kwa darubini kisha inabidi uweke darubini. Lazima uweze kuona kila kitu kwa uwazi.
"Niliwaambia wachezaji jinsi walivyo wazuri, na jinsi tunavyoshukuru kushiriki nao kila siku na kuhakikisha kwamba, tunafurahia kwa imani kubwa kwamba itatokea kwa sababu ni wakati wetu na tunataka kweli."
Arsenal wamemaliza katika nafasi ya pili kwa misimu mitatu iliyopita na hawajashinda taji la ligi Kuu kwa miaka 22.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED