RAIS wa zamani wa Shirikisho la soka la Kimataifa, FIFA, Sepp Blatter amewataka mashabiki 'kujiepusha' na mechi za Kombe la Dunia nchini Marekani mwaka huu, kutokana na mwenendo wa Rais, Donald Trump na utawala wake ndani na nje ya nchi.
Blatter, amekuwa mtu maarufu hivi karibuni katika soka kutilia shaka mwenendo wa Marekani kama nchi mwenyeji katika kupitia chapisho lake ambapo kwenye mtandao wa X aliandika, kombe la Dunia nchini Marekani linatakiwa kususiwa, akiunga mkono maoni ya Wakili, Mark Pieth aliyefanya mahojiano wiki iliyopita na gazeti la Uswisi la Der Bund.
Pieth, wakili wa Uswisi aliyebobea katika uhalifu na mtaalamu wa kupambana na ufisadi, aliongoza Kamati Huru ya Utawala ya kusimamia mageuzi ya FIFA muongo mmoja uliopita.
Blatter alikuwa rais wa FIFA kuanzia mwaka 1998 hadi 2015, alipojiuzuru na kufungiwa kutojihusisha na soka kutokana na tuhuma za ufisadi, uchunguzi uliofanywa na Marekani.
Katika mahojiano yake na gazeti la Der Bund, Pieth alisema, "Tukizingatia kila kitu ambacho tumejadili, kuna ushauri mmoja tu kwa mashabiki, Kaeni mbali na Marekani! Mtaona vizuri zaidi kwenye televisheni zenu."
Katika chapisho lake la X, Blatter alimnukuu Pieth na kuongeza: "Nadhani Mark Pieth, yuko sahihi kuhoji kuhusu Kombe hili la Dunia nchini Marekani.
“Mashabiki wanatakiwa kubakia nchini mwao na wasiende Marekani, maana mwenendo wa rais Trump sio wa kuungwa mkono,” alisema Blatter.
Marekani inaandaa Kombe la Dunia pamoja na Canada na Mexico kuanzia Juni 11 hadi Julai 19 mwaka huu.
Wasiwasi wa jumuiya ya soka ya kimataifa kuhusu Marekani unatokana na msimamo wa rais Trump wa kujitanua kuhusu kutaka kukichukua kisiwa cha Greenland.
Oke Göttlich, mmoja wa makamu wa rais wa shirikisho la soka la Ujerumani, aliliambia gazeti la Hamburger Morgenpost katika mahojiano yake Ijumaa kwamba, wakati umefika wa kufikiria kwa uzito kususia Kombe la Dunia.
Wiki mbili zilizopita, mipango ya usafiri kwa mashabiki kutoka nchi mbili kubwa za soka barani Afrika ilivurugika wakati utawala wa Trump ulipotangaza kutowaruhusu mashabiki kutoka nchi za Senegal na Ivory Coast.
Mashabiki kutoka Iran na Haiti, nchi zingine mbili ambazo zimefuzu Kombe la Dunia, pia wamezuiwa kuingia Marekani.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED