WACHEZAJI waliowahi kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa nyakati tofauti, Fiston Mayele, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na Pape Osmane Sakho wamefunguka kufuatia kiungo Clatous Chama kurejea kwenye klabu ya Simba.
Juzi usiku, Simba ilitangaza kumrejesha Chama, kiungo mshambuliaji raia wa Zambia aliyekuwa akiichezea Singida Black Stars.
Wachezaji hao wameelezea maoni yao kwa Mzambia huyo kurejea ndani ya kikosi cha Simba huku wakimpongeza kwa hatua hiyo na kumtakia heri.
Mayele, staika wa zamani wa Yanga, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo anayeichezea Pyramids ya Misri, ameeleza kufurahishwa kwake, akimtaka kiungo huyo kuendele kuonesha ubora wake katika klabu aliyoizoea na kumpa mafanikio na jina kubwa alilonalo sasa.
"Namba 10 bora amerudi, Mwamba wa Lusaka. Kila la heri kwenye safari yako, endelea kung’ara na kuonesha ubora wako," aliandika Mayele kwenye kurasa yake ya mtandao wa kijamii.
Okwi, raia wa Uganda aliyeichezea Simba kwa nyakati tatu tofauti kama Chama, alimpongeza kiungo huyo kwa kurejea kwenye klabu iliyompatia heshima akimkaribisha nyumbani.
"Karibu kaka, karibu tena nyumbani," aliandika Okwi ambaye kwa sasa anakipiga kwenye klabu ya Kiyovu Sports ya Rwanda.
Sakho, winga wa zamani wa Simba raia wa Senegal, anayeichezea Raja Casablanca ya Morocco kwa sasa, naye ameonesha kufurahia usajili huo akimwambia kuwa timu aliyokwenda ndiyo ya ndoto yake na inayomstahili.
Straika wa zamani wa Simba Kagere, amempongeza na kumkaribisha tena Msimbazi.
"Karibu tena Msimbazi," aliandika straika huyo raia wa Rwanda, huku beki wa kati za zamani wa Simba na Azam, Wawa, akimpa hadhi ya unahodha,"karibu nyumbani nahodha wetu."
Hii ni mara ya tatu kwa Chama kurejea klabu ya Simba, huku usajili huyo ukipokelewa kwa hisia tofauti na wanachama na mashabiki wa timu hiyo.
Kocha Mkuu Steve Barker, amesema ujio wa Chama utaongeza nguvu kwenye kikosi chake kwa sababu ni mmoja wa wachezaji bora na wenye uzoefu.
Akizungumza jana alfajiri wakati kikosi hicho kikiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa safari ya kwenda nchini Tunisia kuivaa Esperance Jumamosi ijayo, katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kocha huyo amesema amefurahishwa na usajili wa Chama na wenzake kwani utaisaidia timu kuimarika na kuleta ushindani kwa wachezaji wengine.
Chama alijiunga kwa mara ya kwanza na Simba mwaka 2018 hadi 2021 alipouzwa kwenye klabu na RS Berkane ya Morocco, lakini alirejea tena Msimbazi mwaka 2022 alipodumu mpaka mwaka 2024 alipokwenda kwa watani zao wa jadi, Yanga.
Akiwa Yanga alicheza kwa msimu mmoja tu, ulipomalizika alijiunga na Singida Black Stars mwanzoni mwa msimu huu, kabla ya kuibukia tena Msimbazi kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.
Wakati huo huo, Simba pia imetangaza kumsajili golikipa Mahamadou Tanja Kassali, kutoka AS Fan ya Niger.
Kipa huyo alikuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Niger, kilichoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), zilizofanyika mwaka jana katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED