slot gacor
slot gacor
slot gacor
Ibenge: Azam bado tuna kazi ya kufanya | Nipashe

Ibenge: Azam bado tuna kazi ya kufanya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:10 PM Jan 27 2026
news
Picha Mtandao
Ibenge: Azam bado tuna kazi ya kufanya

LICHA ya ushindi wa mabao 2-1 walioupata juzi dhidi ya Nairobi United ya Kenya, Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema kikosi chake bado kina kazi kubwa ya kufanya kuweza kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuwasajili wakitokea Nairobi, Kenya, Ibenge, alisema kuna kazi kubwa ya kufanya kukiimarisha kikosi chake kwa mashindano hayo ya ugumu wake.

"Bado nina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha timu yangu inaingia hatua ya robo fainali, tuna mchezo wa marudiano dhidi ya Nairobi United, ni lazima tubadilike na kuimarika zaidi," alisema Ibenge. 

Akizungumzia mchezo uliopita, Ibenge, alisema ulikuwa mchezo mgumu lakini wachezaji wake walijitahidi kufuata maelekezo yake na kufanikiwa kuvuna pointi tatu ugenini.

Alisema anajivunia kwa kiasi kikubwa wachezaji wake hao kutokana na yale wanayoyafanya nje na ndani ya uwanja kwa maslahi ya timu yao. 

Alisema mchezo ulikuwa na upinzani mkubwa isipokuwa wamepambana na kuweza kurudi nyumbani na pointi tatu. 

"Malengo yetu yalikuwa kupata pointi tatu ambazo tumezipata, kwa sasa tunaelekeza nguvu kwenye mchezo wetu ujao wa marudiano," alisema Ibenge.

Aidha, aliwashukuru mashabiki wa klabu hiyo kwa ushirikiano waliouonesha wakiwa ugenini ambapo baadhi yao walisafiri kwenda kuwashangilia.

Kwa upande wake, nahodha wa timu hiyo, Himid Mao, alisema matokeo waliyoyapata Nairobi wanayaacha nyuma na sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye mchezo wa marudiano.

"Ushindi tulioupata Nairobi umetufanya tuzidi kupata nguvu ya kujituma zaidi katika mchezo wetu wa marudiano tutakaoucheza wikiendi hii New Amaan Zanzibar, akili na nguvu zetu tunazielekeza kwenye mchezo huu, tunataka kupata pointi zote tatu" alisema Mao. 

Ushindi wa juzi sasa umeifanya Azam kufikisha pointi tatu baada ya kucheza michezo mitatu kwenye kundi lao la michuano hiyo.