WAKATI ikiongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya JKT Tanzania inaongoza pia kwa kuwa na kadi nyingi za njano mpaka kufikia sasa.
Maafande hao wanaongoza ligi kwa pointi 17 lakini pia wana kadi za njano 22 zilizotolewa katika michezo 10 ambayo wamecheza, huku Yanga ikiwa na kadi moja tu ya njano.
Mbali na kuwa na kadi nyingi za njano, JKT Tanzania ndiyo timu yenye sare nyingi kwenye ligi ikiwa nazo tano huku pia ikiwa na mabao mengi zaidi ya kufunga ikifanya hivyo mara 12, sawa na Yanga.
Kwa mujibu wa takwimu za michezo la dawati la Nipashe, timu inayoshika nafasi ya pili kwa kuzawadiwa kadi nyingi za njano ni Namungo, ikipata idadi ya kadi 14 katika michezo nane iliyocheza wakati Dodoma Jiji ikiwa nafasi ya tatu, ikipata kadi 13 kwa michezo minane iliyocheza mpaka sasa.
Takwimu zinaonesha kuwa nafasi ya nne inakwenda kwa timu za Fountain Gate na TRA United ambazo kila mmoja imeonywa mara 11 kwa kadi za njano.
Hata hivyo, Fountain Gate ina idadi hizo za kadi ikicheza michezo 10, huku TRA United ikishuka dimbani mara saba tu.
Timu zilizo nafasi ya tano kwa kadi nyingi za njano ni Mashujaa FC yenye kadi 10 baada ya michezo tisa iliyocheza na Mbeya City ikiwa na idadi kama hiyo kwa michezo 10 iliyocheza sawa na Prisons ambayo imecheza michezo saba.
Mtibwa Sugar ina kadi tisa za njano ikiwa imecheza michezo minane, Pamba Jiji na KMC kila moja ikipata kadi nane za njano baada ya kucheza michezo tisa, Coastal Union yenyewe imelimwa kadi saba za njano ikicheza michezo minane.
Singida Black Stars na Azam FC zina kadi tano za njano mpaka sasa, kila moja ikicheza michezo mitano wakati Simba imepata kadi nne za njano kwa michezo mitano iliyocheza.
Timu iliyopata kadi chache zaidi kwenye Ligi Kuu mpaka sasa ni Yanga, ikioneshwa kadi moja tu kwa michezo sita iliyocheza mpaka sasa.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED