slot gacor
slot gacor
slot gacor
Karabaka, Peter hatari mabao ndani ya boksi | Nipashe

Karabaka, Peter hatari mabao ndani ya boksi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:26 AM Jan 26 2026
news
Picha Mtandao
Wachezaji wa kikosi cha JKT Tanzania, Salehe Karabaka na Paul Peter.

WACHEZAJI wawili wa JKT Tanzania, Salehe Karabaka na Paul Peter wanaongoza kwa kufunga mabao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini pia ndiyo vinara wa kupachika mabao ndani ya eneo la hatari.

Bao pekee alilofunga Jumanne iliyopita likiipa JKT Tanzania ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars lilimfanya Karabaka anayeichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Simba kufikisha jumla ya mabao matano akimfikia mchezaji mwenzake, Peter.

Wakati wachezaji hao wakiwa na mabao matano wanaongoza pia kwa kufunga mabao wakiwa ndani ya eneo la hatari, kila mmoja akifunga manne.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana na Bodi ya Ligi, Karabaka na Peter wamefunga mabao manne wakiwa ndani ya boksi, huku kila mmoja akifunga bao moja nje ya eneo la hatari.

Takwimu zinaonesha nafasi ya pili inashikiliwa na wachezaji wanne ambao wamepachika mabao ndani ya eneo la hatari mpaka sasa.

Wachezaji hao ni Jonathan Sowah wa Simba akipachika mabao yote matatu aliyonayo ndani ya eneo la hatari, Fabrice Ngoy wa Namungo, Prince Dube wa Yanga na Feisal Salum wa Azam FC.

Wakati huo huo, Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea tena kesho kwa michezo miwili ambapo TRA United itakuwa nyumbani kwenye uwabnja wa Ali Hassan Mwinyi kucheza dhidi ya Namungo.

Mechi hiyo itapigwa saa 10:00 jioni, wakati saa 1:00 usiku kutakuwa na mchezo mwingine kati ya Coastal Union itakapokipiga dhidi ya KMC.