ALIYEKUWA golikipa wa Yanga na Timu ya Taifa (Taifa Stars), Manyika Peter, anatarajiwa kuzikwa leo kuanzia saa 9:00 mchana katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Msemaji wa familia, Lucas Mgweno, aliliambia gazeti hili jana, taratibu na maandalizi kwa ajili ya kukamilisha safari ya mwisho ya Manyika, yamekamilika.
"Jana (juzi) jioni tulikaa kikao cha familia na kwa pamoja tukakubaliana tumpumzishe kesho (leo) majira ya saa tisa jioni kwenye makaburi ya Kinondoni, tunaomba wadau wa michezo wajumuike nasi katika kukamilisha safari hii ya mwenzetu," alisema Mgweno.
Alisema ibada ya kumsalia na kumuaga marehemu itafanyika kuanzia saa 7:00 mchana katika Kanisa Katoliki Buricheka (Malamba Mawili- Mbezi).
“Tunawashukuru wadau wote kwa ushirikiano wanaotupatia ikiwamo uongozi wa Klabu ya Namungo ambayo marehemu alikuwa anafanya kazi, wamekuwa karibu na sisi kuanzia wakati wa ugonjwa mpaka umauti unamkuta,’’ Mgweno alisema.
Katibu Mkuu wa Namungo, Ally Suleiman, alisema wamepoteza mwalimu ambaye alifanya ‘mapinduzi makubwa’ katika timu yao hasa kwa upande wa walinda mlango.
“Nipo njiani ninakuja Dar es Salaam kwa ajili ya kuungana na familia ya Manyika katika kipindi hiki kigumu cha kumpoteza mwalimu wetu, "alisema Suleiman.
Alisema Namungo imempoteza mtu ambaye walikuwa wanamtegemea na kumwamini katika majukumu yake.
“Alikuwa ni mwalimu ambaye anapenda kufundisha vijana mbalimbali ili wafuate nyayo alizokuwa nazo wakati alipokuwa anacheza, hakika tumepata pigo,” alisema katibu huyo.
Juma Mgunda, Kocha Mkuu wa Namungo, ameliambia gazeti hili kifo cha Manyika kimemwachia upweke kwa sababu mbali na kazi, marehemu alikuwa ni rafiki na mshauri wake.
"Ameniachia ukiwa, kila mara nilikuwa naye, lakini hatupaswi kumlaumu Mungu, kikubwa ni kumwombea," alisema Mgunda.
Manyika pia aliwahi kuitumikia Mtibwa Sugar ya Manungu, Morogoro na klabu mbalimbali za nje ya Tanzania.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED