slot gacor
slot gacor
slot gacor
Simba: Bado haijaisha | Nipashe

Simba: Bado haijaisha

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:48 AM Jan 26 2026
news
Picha Mtandao
Kiungo wa Simba, Maurice Abraham (kushoto) akiwania mpira na mchezaji wa Esperance de Tunis kwenye mchezo wa Kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika juzi usiku, kwenye uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi nchini Tunisia. Simba ilifungwa bao 1-0.

PAMOJA na kupoteza michezo mitatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, klabu ya Simba imesema haitokata tamaa kupigania pointi tisa zilizo ndani ya uwezo wao ili kujua hatma yao kwenye Kundi D.

Akizungumza jana, siku moja tu baada ya kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Eperance de Tunis, katika mchezo uliopigwa uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi, nchini Tunisia, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo Ahmed Ally, amesema ameonana na kocha Steve Barker na wachezaji wa timu hiyo mara baada ya mechi na kumweleza jinsi walivyohuzunika.

"Tumebakiwa na nafasi moja ya dhahabu, nayo ni mechi ya marudiano nyumbani, Februari Mosi, ambayo ni Jumapili ijayo.

Namna ambavyo tumecheza, namna ambavyo wachezaji wetu wamepambana inatia matumaini makubwa ya kufanya vizuri mechi tatu za mwisho

Hatukati tamaa, mechi tatu za mwisho ni halali yetu bado tuna akiba ya alama tisa za kupigania, sasa tunaianza upya safari yetu ya kufukuzia pointi hizi," alisema Ahmed.

Alisema baada ya mchezo kumalizika alikwenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kukutana na kocha Barker pamoja na wachezaji ambao walionekana kuwa na huzuni lakini iliyochanganyika na matumaini.

"Wachezaji wameniambia bado hatujainamisha vichwa chini, wanayo matumaini ya kufanya vizuri kwenye kundi letu japo ni ngumu kwa sababu ni lazima wawe pia wanasikilizia matokeo ya mechi zingine, lakini wamesema wanalazimika kupita njia hiyo hiyo ngumu kufika safari. Wameniambia niwaambie wanachama na mashabiki kuwa Simba hajafa, amejeruhiwa tu," alisema Meneja Habari huyo.

Simba imebakisha mechi tatu dhidi ya Esperance itakayopigwa, Februari Mosi, uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Februari 6 inatarajiwa kwenda Angola kucheza dhidi ya Petro de Luanda kabla ya kumaliza mechi zake za Kundi D dhidi ya Stade Malien, Februari 13, jijini Dar es Salaam.

Timu hiyo imepoteza michezo yote mitatu iliyocheza na kujikuta ikiburuza mkia kwenye Kundi D huku Esperance ikiongoza kundi kwa pointi tano, Petro de Luanda na Stade Malien zilizotarajiwa kucheza jana zina pointi nne kila moja.