WAKATI kikosi cha Simba kimewasili salama nchini Tunisia, uongozi wa timu hiyo umetamba timu yao 'imezaliwa upya' kutokana na kukamilisha usajili wa wachezaji wapya wanne katika kipindi hiki cha dirisha dogo.
Simba imetua katika Jiji la Tunis kwa ajili ya mechi ya raundi ya tatu ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa keshokutwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania.
Ndani ya saa 48, Simba ilitangaza kukamilisha usajili wa wachezaji wapya wanne ambao ni Nickson Kibabage, Ismael Toure, kipa, Djibrille Kessah na kiungo Mzambia, Clatous Chama.
Akizungumza na Nipashe jana jijini hapa, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema usajili ambao wameufanya utarejesha ubora na heshima ya kikosi chao katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki.
Ahmed alisema usajili wao umefanyika kwa kuzingatia mapendekezo ya benchi la ufundi ambalo kwa sasa liko chini ya Kocha Mkuu, Steve Barker, raia wa Afrika Kusini.
Alisema wachezaji wote hao wameshajiunga na timu na wanatarajia kuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani Jumamosi kuwakabili wenyeji Esperance de Tunis.
"Timu yetu imezaliwa upya, tunajua ilikuwa wapi na tunalenga kufika wapi, wachezaji ambao wamesajiliwa ni wa daraja la juu na wako tayari kwa mapambano, tulizingatia mambo mengi kabla ya kuwasajili," alisema Ahmed.
Naye Chama ambaye juzi alicheza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na Singida Black Stars aliliambia gazeti hili amerejea nyumbani na anafahamu malengo ya Simba wakati wote.
"Nimerejea Simba, ninajua nini Simba inataka," alisema kwa kifupi nyota huyo ambaye pia amewahi kuichezea Yanga.
Wakati huo huo, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, ambaye kikosi chake kipo nchini Misri kucheza dhidi ya Al Ahly, amesema hawaendi kucheza mfumo wa kuzuia badala yake watashambulia ili kupata ushindi katika mchezo wa raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kesho kwenye uwanja wa Kimataifa wa Cairo kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania.
Akizungumza jana, kocha huyo amesema hawatobadilisha aina yao ya uchezaji katika mechi hiyo ya ugenini, badala yake watataka kutawala mpira na kushambulia ili kutafuta ushindi kwani wanazihitaji zaidi pointi tatu.
Hata hivyo amekiri kuwa anakwenda kucheza na timu kubwa na bora barani Afrika, lakini wanakwenda kwa kujiamini.
"Itakuwa mechi ngumu kwa kweli, Al Ahly ni timu kubwa, bora, kongwe na klabu ya kihistoria barani Afrika, pia inakuwa na nguvu maradufu inapocheza nyumbani, lakini pamoja na hayo wachezaji wangu wana morali na watafanya kile ambacho tutaelekezana, tunakwenda tukiwa tunajiamini," alisema Goncalves.
Kocha huyo alisema watacheza mchezo wao ule ule wa kushambulia na hawatakaa nyuma kwa kuwa wanataka kushinda na kuondoka na pointi tatu baada ya dakika 90.
Watani wa jadi jana alfajiri waligongana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ambapo Yanga alikuwa akielekea Misri kuwafuata Al Ahly kwa ajili ya mchezo wa raundi ya tatu utakaochezwa kesho katika jiji la Alexandria nchini humo huku Simba ikiwafuata Esperance nchini Tunisia.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED