slot gacor
slot gacor
slot gacor
Singida BS mechi tano bila ushindi | Nipashe

Singida BS mechi tano bila ushindi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:59 PM Jan 22 2026
news
Picha Mtandao
Singida BS mechi tano bila ushindi

KIPIGO cha bao 1-0 ilichokipata Singida Black Stars juzi dhidi ya JKT Tanzania kimeifanya timu hiyo kucheza michezo mitano ya Ligi Kuu bila kupata ushindi wowote mpaka sasa.

Bao la winga anayechezea JKT Tanzania kwa mkopo akitokea Simba, Salehe Karabaka dakika ya 81, liliwarudisha tena maafande hao kileleni mwa msimamo katika mchezo uliopigwa jana usiku, Uwanja wa KMC Complex, ikiiengua Yanga iliyokaa kileleni kwa siku moja tu.

Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kuchezwa usiku kwenye uwanja huo baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa, ikiwamo kufungwa taa.

Singida imeendelea kusotea ushindi wa kwanza tangu ilipoifunga Mashujaa FC bao 1-0, Septemba 30 mwaka jana.

Baada ya hapo timu hiyo imecheza michezo mitano ya ligi bila ushindi, ikipoteza miwili na sare tatu.

Mbali na kupoteza jana kwa bao 1-0, pia ilichapwa mabao 3-1 na TRA United, Desemba 6 mwaka jana.

Aidha, ilitoka suluhu dhidi ya Azam FC kabla ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya timu za Pamba Jiji na Dodoma Jiji.

Mabingwa Watetezi, walikaa juu ya msimamo baada ya kupata ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa FC na kufikisha pointi 19, lakini ushindi wa maafande umewarejesha juu kwa kufikisha pointi 20.

Hata hivyo, JKT Tanzania imecheza michezo minne zaidi ya Yanga iliyoshuka dimbani mara saba msimu huu.

Bao hilo pia linamfanya Karabaka kukaa juu ya orodha ya wafungaji wa mabao Ligi Kuu, akifikisha mabao matano sawa na mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Paul Peter.