TANZANIA ikitarajia kuwa mwenyeji wa fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), inakabiliwa na tatizo la kipa, kutokana na aliyekuwa mlinda mlango chaguo la kwanza wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Yakoub Suleiman, kupata majeraha.
Yakuob ambaye ni nyota wa Simba, alishindwa kuendelea kuitumikia Taifa Stars katika mechi za mashindano ya AFCON yaliyomalizika hivi karibuni baada ya kuumia akiwa mazoezini na nafasi yake kuchukuliwa na Zuberi Foba wa Azam na Hussein Masalanga wa Singida Black Stars.
Kucheza katika viwanja vibovu na vyenye nyasi bandia vinatajwa kuongeza hatari kwa wachezaji hasa magolikipa, jambo linalowasababishia kuteleza na kupata majeraha ya vifundo na magoti.
Kadhalika, vifaa visivyofaa kama vile glovu, viatu au mavazi yasiyo sahihi, vinatajwa kuchangia hatari kwa wachezaji hao na kupunguza ulinzi wa mwili.
Mtaalamu wa Misuli wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH-Mloganzila), Aloyce Bwana, aliliambia Nipashe jana, sababu hizo ni baadhi zinawazofanya walinda mlango kuumia mara kwa mara.
Bwana alisema wachezaji wa mpira wa miguu hasa makipa wamekuwa miongoni mwa waathirika wakubwa wa majeraha yanayotokana na michezo, na baadhi kusababisha kukaa muda mrefu benchi wakisubiri kupona.
“Walinda lango (golikipa) ni miongoni mwa wachezaji wanaokumbwa na majeraha mara kwa mara katika mchezo wa mpira wa miguu.
Nafasi yao ni ya kipekee na inahitaji matumizi makubwa ya mikono, kuruka, kudondoka, kupiga mbizi na kukabiliana na mashambulizi ya moja kwa moja.
Zipo takribani sababu 21 zote zinazochangia majeraha kwa walinda mlango, bila kufupisha, ili kutoa uelewa mpana wa tatizo hili,” alisema mtaalamu huyo wa mazoezi.
Alisema pia kukosa vifaa vya kinga, kutokutumia vifaa vya ulinzi wa magoti, viwiko na mabega huongeza majeraha kwa wachezaji hao moja kwa moja.
“Uchovu na ukosefu wa mapumziko. Ratiba ngumu ya mazoezi na kucheza mechi bila mapumziko ya kutosha huathiri uwezo wa mwili kujirekebisha.”
Kipa na kocha mkongwe nchini, Juma Pondamali, amesema anashangazwa na makipa wa siku hizi kuumia wakati kuna sheria nyingi zinawalinda.
Pondamali pia alisema viwanja vya sasa vina ubora tofauti na ilivyokuwa wakati yeye anacheza lakini walifanya kazi yao vyema.
"Makipa tuliweza kudaka hata mwaka mzima bila kuumia, labda uumizwe na mchezaji wa timu pinzani, lakini siyo viwanja licha ya havikuwa na ubora kama ilivyo sasa. Wakati huo viwanja vilikuwa vigumu sana, si Dar es Salaam wala mikoani, nyasi zinachoma, nashangaa makipa wengi wa sasa wanaumia wakati tunaona wanacheza kwenye viwanja bora, nyasi zinamwagiwa maji, tumeona uwanja mkubwa kama wa Benjamin Mkapa, umechimbwa na kuwekwa udongo mpya na nyasi za kisasa," alisema Pondamali.
Aliongeza wakati wao wakicheza makipa wengi walivaa 'tracksuits' na jezi za mikono mirefu tofauti na sasa ambapo wanadaka na jezi za mikono mifupi na bukta.
"Huku pembeni ya mapaja 'tracksuits' zilikuwa na sponji ambazo zilitusaidia hata tukiruka tusiumie au kupata vidonda, makipa wa sasa wao hawana hilo, labda kwa sababu wanacheza kwenye viwanja bora," Pondamali aliongeza.
Kipa huyo pia alikumbusha wao hawakuwa wanavaa 'glovu', walikuwa wanadaka mikono mitupu.
“Nimeshakorofishana na waamuzi sana kuhusu jambo hilo, nikaona bila ubabe 'hutoboi', nashukuru kwa sasa ni kama wameliona na sheria zimebadilishwa. Lakini kama ingekuwepo nadhani makipa majeruhi wangeongezeka zaidi," alisema.
Pondamali amekubaliana na madaktari huenda nyasi bandia nazo zikawa zinachangia, kuongezeka kwa majeruhi kwa sababu zamani hakukuwa na viwanja vya aina hiyo.
Mpaka sasa rekodi ya makipa majeruhi kwa msimu huu kwa Simba ni Moussa Camara, aliyefanyiwa upasuaji na Yakoub, ambaye bado anaendelea na matibabu.
Aboutwalib Mshery wa Yanga na Aishi Manula, alipokuwa Simba kwa nyakati tofauti walifanyiwa upasuaji ili kupona jeraha na goti baadaye kurejea tena dimbani.
Djigui Diarra wa Yanga na Mussa Mbise wa Prisons, pia waliwahi kuuguza jeraha la goti, lililopelekea kukaa nje kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED