KOCHA wa Liverpool, Arne Slot amesema anatarajia, Andy Robertson atabaki klabuni hapo baada ya mwisho wa dirisha hili la uhamisho la Januari.
Robertson amejikuta akiwa beki wa kushoto wa chaguo la pili tangu kuwasili kwa Milos Kerkez msimu wa joto na Tottenham Hotspur inaaminika kuwa inampango wa kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Scotland.
Hata hivyo, Slot amedai kwamba, mlinzi huyo ana jukumu la kucheza klabuni hapo na hatarajii aondoke mwezi huu.
"Robby ni sehemu ya timu. Amekuwa sehemu ya klabu hii kwa miaka mingi. Ninafurahi kuwa naye," alisema Slot akinukuliwa na ESPN.
"Ni vizuri kwamba anapatikana kwa sababu hilo ni muhimu sana kwetu kwa sasa. Atakuwa sehemu ya timu na hakuna kilichotokea kutoka upande wangu.
"Ni vigumu kusema chochote cha uhakika katika ulimwengu huu, lakini natarajia atabaki."
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED