WADAU wa soka nchini wamesikitishwa na kifo cha aliyekuwa mlinda mlango wa zamani wa timu ya Taifa na Yanga, Peter Manyika aliyefariki jana asubuhi jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili wadau hao walisema tasnia ya michezo imeondokewa na nguzo muhimu.
Soud Slim, ambaye ni kocha wa magoli wa timu za vijana za Yanga, alisema amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Manyika na kumwelezea kuwa alifanya mambo makubwa kwa Taifa kutokana na juhudi alizokuwa nazo katika mpira.
"Peter Manyika alikuwa miongoni mwa wachezaji na walimu wazuri ambao amefanya mambo makubwa kwa Taifa letu katika tasnia ya mpira," alisema Slim.
Naye kocha wa zamani wa Yanga na timu ya taifa 'Taifa Stars', Boniface Mkwasa, alisema Manyika ameacha pengo kubwa katika tasnia ya mpira na anaungana na familia yake kuomboleza kifo chake.
"Msiba huu umenishtua sana, nilishawahi kufanya naye kazi, alikuwa mtu ambaye anapenda kujifunza na kushirikiana na kila mmoja bila kubagua mtu yeyote," alisema Mkwasa.
Idd Moshi ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Yanga na ni rafiki wa karibu na marehemu, Manyika, alikuwa akisumbuliwa na uvimbe tumboni pamoja na tatizo la kupungukiwa damu.
Alisema Manyika alikuwa amelazwa katika hospitali ya 'St Bernard' iliyopo Manzese jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu, lakini alifariki jana asubuhi.
"Mwili wake umehifadhiwa kwenye hospitali ya Mwananyamala huku tukisubiri taratibu za mazishi," alisema Moshi.
Alisema kwa sasa msiba upo nyumbani kwa marehemu, Mbezi Maramba mawili.
Mtoto wa mchezaji huyo, Manyika Peter, ambaye aliwahi kuidakia Simba, alithibitisha kifo cha baba yake, akisema alifariki jana asubuhi.
"Baba kafariki leo (jana) alfajiri, msiba upo nyumbani Mbezi, kwa sasa ni ngumu kusema vitu vingi bado sijatulia,"amesema Manyika Jr.
Kwa upande wake, Msemaji wa familia ambaye ni shemeji wa marehemu, Lucas Mgweno, alisema walitegemea jana jioni familia kukutana kwa ajili ya kupanga taratibu za mazishi.
"Leo (jana) jioni tutakaa kikao cha familia ambacho kitaamua siku ya mazishi nitatoa taarifa rasmi ya mazishi baada ya kikao hicho," alisema Mgweno.
Alisema Marehemu alikuwa akisumbuliwa na tumbo kwa muda mrefu na madaktari walipambana kuokoa maisha yake lakini ilishindikana na jana asubuhi akaaga Dunia.
Manyika, alianza kujulikana akiwa katika klabu ya Mtibwa Sugar aliyoipandisha Ligi Kuu kwa mara ya kwanza mwaka 1996, kabla ya kuhamia Sigara FC ya Dar es Salaam ambapo usajili huo ulileta utata kiasi cha timu hiyo aliyohamia kushushwa daraja.
Ilionekana kuwa Sigara ilikiuka utaratibu katika kumsajili kutoka Mtibwa, hivyo ilipokwa pointi zote ambazo Manyika alicheza na kusababisha timu hiyo ishuke daraja mwaka 1997.
Mwaka 1998, manyika alijiunga na Yanga ambako aliichezea kwa mafanikio makubwa.
Aliidakia hadi mwaka 2001 alipokwenda nchini Botswana kucheza soka ya kulipwa hadi mwaka 2004 akarejea nchini na kujiunga na tena na Mtibwa Sugar alikocheza hadi alipostaafu mwaka 2006.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED