SIKU chache baada ya kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya Al Ahly katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo watashuka dimbani kucheza dhidi ya Dodoma jiji huku Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Patrick Mabedi akisema wanataka ushindi ili kuwarejeshea furaha mashabiki wake.
Akizungumza kuelekea kwenye mchezo huo utakaochezwa saa 1:00 usiku, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Mabedi, amesema wanataka kuwarejeshea furaha wanachama na mashabiki wa Yanga kabla ya mchezo mwingine dhidi ya Al Ahly, unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi ijayo kwenye uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
"Tunakwenda kucheza dhidi ya Dodoma Jiji, tunahitaji kushinda mchezo huu. Tunahitaji kushinda ili kuwarejeshea furaha mashabiki wetu na kuwaweka tayari kwa ajili ya kutushangilia na kutupa hamasa kwenye mchezo wetu ujao dhidi ya Al ahly.
Lakini haitokuwa rahisi kutokana na uchovu wa wachezaji wetu. Tumesafiri kwa umbali mrefu sana kutoka Misri, hatuna cha kufanya ni lazima tuingie uwanjani. Kwa bahati mzuri tunao wachezaji ambao hawajatumika sana kwa hiyo tuko tayari," alisema raia huyo wa Malawi.
Licha ya kufungwa mabao 2-0 nchini Misri katika mchezo wa Kundi B, Yanga itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kutoa kipigo cha mabao 6-0 kwa Tanzania Prisons katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu kabla ya kuelekea jijini Alexandria.
Ni mchezo ambao kama itashinda itapanda juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Yanga ina pointi 19, ikiwa imecheza michezo saba huku vinara wa ligi hiyo, JKT Tanzania ikiwa na pointi 21 ikicheza michezo 12 mpaka sasa.
Kocha wa Dodoma Dodoma Jiji, Amani Josiah, amesema mechi hiyo ya leo itakuwa mgumu kwa pande zote mbili.
Amesema Yanga ni timu kubwa kiasi kwamba hata wachezaji wao wa akiba ambao hawajacheza mechi dhidi ya Al Ahly ni wazuri pia.
"Itakuwa mechi kubwa, watakuja kwa hasira kwa sababu wamepoteza dhidi ya Al Ahly, tutaingia kwa kuiheshimu Yanga kwa sababu ndiyo mabingwa wa sasa, ndiyo wanaolitetea kombe na moja kati ya timu bora kwenye ligi yetu.
Hatutoshindana nao, tutajiangalia sisi tutaingiaje dhidi ya timu kubwa," alisema Josiah.
Dodoma jiji ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 10 katika michezo 10 iliyocheza.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED