slot gacor
slot gacor
slot gacor
Yanga yaanza jeuri, Simba yaita mashabiki | Nipashe

Yanga yaanza jeuri, Simba yaita mashabiki

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:37 AM Jan 29 2026
news
Picha Mtandao
Kocha Msaidizi wa Yanga, Patrick Mabedi, kushito.

WAKATI Kocha Msaidizi wa Yanga, Patrick Mabedi, amesema timu yao ilistahili kupata ushindi ‘mnono’ katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji iliyochezwa juzi, Simba imewataka mashabiki wake kujitokeza kwa wingi leo kushuhudia burudani ikiwaalika Mashujaa FC kutoka mkoani, Kigoma.

Yanga ilipata ushindi wa mabao 3-1 ilipokutana na Dodoma Jiji juzi na kufikisha pointi 22, zilizowafanya wakae kileleni katika msimamo wa ligi hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mabedi, alisema hajaridhika na idadi ya mabao ambayo wamepata katika mchezo huo kutokana na nafasi nyingi za wazi zilizotengenezwa katika mchezo huo. 

"Nilisema kabla ya mchezo mechi itakuwa ngumu, ukitaka kujua ugumu wake angalia leo (juzi), tumeruhusu bao katika mchezo wa Ligi Kuu. Nadhani ni mara ya pili sasa kufanya hivyo. Tulipata nafasi nyingi sana, lakini hatukutumbukiza mpira ndani ya wavu, hili ni tatizo.

Wapinzani wetu walitusubiri nyuma na wakatushambulia kwa kushtukiza na walikuwa hatari sana kipindi cha kwanza, baadaye tukalipatia ufumbuzi, tulifanya mabadiliko na kutowapa tena nafasi hiyo.

Mwisho wa siku lengo letu lilikuwa ni kushinda na kupata pointi tatu na ndilo tulilolifanya," alisema Mabedi, ambaye ni raia wa Malawi.

Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, aliliambia gazeti hili kikosi chao kimeshawasili Zanzibar tayari kwa mchezo wa raundi ya nne wa Kundi B wa mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly kutoka Misri utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja New Amaan Complex.

Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amewataka mashabiki na wanachama wa timu hiyo ‘kumiminika’ kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo leo ili kushuhudia nyota wapya waliosajiliwa ambao wamekibadilisha ubora wa kikosi hicho.

"Tunatakiwa kucheza kwa ari na ufanisi na hili litafanyika kwa sababu kuna mabadiliko kadhaa kikosini, kuna baadhi ya wachezaji wameondoka na wengine wameingia kikosini, wako vizuri na watu wote wanatakiwa kuja kuwaona nyota hawa wakiwa katika viwango bora sana.

Nawaomba mashabiki waje kwa wingi uwanjani kushuhudia hilo, nadhani watakuwa wameona kiwango ambacho kimeoneshwa na timu yao katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Esperance, kikosi kinaendelea kuimarika siku hadi siku," alisema Barker.

Kocha huyo alisema amewaandaa wachezaji wake katika mchezo wa leo wapambane ili kuhakikisha hawapotezi pointi na kutowadharau wapinzani.

"Tunakwenda kuhakikisha hatupotezi mechi tena ndani ya uwanja, ligi ni ngumu, imeonekana hivyo, kwa hiyo wachezaji hawapaswi kuwadharau wapinzani kwa namna yoyote ile," kocha huyo alisema.

Salum Mayanga, Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, amesema wamerejea tena Dar es Salaam na hawatarajii kurudia makosa waliyoyafanya walipokutana na Yanga, ambapo walichapwa mabao 6-0.

"Tumerudi tena Dar, tumejaribu kufanya masahihisho ya makosa tuliyoyafanya katika mchezo uliopita. Tutacheza kwa tahadhari kuwaheshimu Simba na kwa utulivu, tunategemea utakuwa mchezo wa kimbinu zaidi, jambo zuri tumewaona katika michezo yao miwili, ule wa kimataifa dhidi ya Esperance na wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar," Mayanga alisema.