slot gacor
slot gacor
slot gacor
Yanga yaigeukia Dodoma Jiji | Nipashe

Yanga yaigeukia Dodoma Jiji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:07 AM Jan 26 2026
news
Picha Mtandao
Kikosi cha YangaSC

BAADA ya kukumbana na kipigo cha mabao 2-0 mbele ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wa raundi ya tatu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga wamepania kumaliza hasira zao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kesho dhidi ya Dodoma Jiji.

Akizungumza jana mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema ili kurejesha nguvu na morali kwa wachezaji na mashabiki kuelekea kwenye mchezo wa raundi ya nne Kundi B dhidi ya Al Ahly utakaochezwa Jumamosi ijayo kwenye uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ni lazima wapate ushindi kwenye mchezo huo wa kesho.

"Tumerejea salama, ni kweli tulikwenda kupambana ili kupata matokeo mazuri, lakini bahati haikuwa upande wetu. Al Ahly ni timu ambayo ni vigumu sana kupoteza nyumbani kwao hata ukiangalia rekodi zao, mara chache sana wanapoteza. Kabla ya kurudiana nao Jumamosi tunauangalia kwanza mchezo wetu dhidi ya Dodoma Jiji.

Tuna mchezo wa ligi kwenye uwanja wa KMC Complex dhidi ya Dodoma Jiji, nadhani tukishinda utaturudishia ari na nguvu kuelekea mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa," alisema Kamwe.

Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku, ambapo kwa mara ya kwanza Yanga itacheza mechi hiyo usiku katika uwanja huo ambao unauitumia kama uwanja wa nyumbani.

Hiyo itakuwa mara ya pili kwa mechi ya Ligi Kuu kuchezwa usiku katika uwanja huo iliopo maeneo ya Mwenge, mara ya kwanza ilikuwa mchezo kati ya Singida Black Stars dhidi ya JKT Tanzania uliopigwa Januari 20 mwaka huu ukaisha kwa maafande kushinda bao 1-0.

Akizungumzia kupoteza mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema kwa jinsi hata iliivyoonekana kwenye upangaji wa kikosi walikwenda Misri kwa ajili ya kusaka pointi moja ambayo kwa bahati mbaya waliikosa.

Katika mchezo huo, Kocha Mkuu, Pedro Goncalves alipanga mabeki watatu wa kati ambao ni Dickson Job, Ibrahim Hamad 'Bacca' na Bakari Mwamnyeto, pembeni kukiwa na Israel Mwenda na Shadrack Boka, waliokuwa wakilindwa na Mohamed Domaro na Duke Abuya, ikionesha kuwa walikuwa kwenye mfumo wa kujilinda zaidi.

"Si aina ya matokeo ambayo yametufurahisha lakini ndiyo soka.

Tusijidanganye Al Ahly si timu dhaifu, tusijidangaye, maana naona kwenye mitandao baadhi ya watu wanasema kama kwao tumecheza vile basi kwetu tutawafunga kirahisi, tunatakiwa tujiandae haswa, wale jamaa wanacheza mechi kwa ufundi na mkakati wa mechi husika, tulikwenda kwao tukihitaji sare, lakini wakang'amua hilo, tumejitahidi sana lakini tukashindwa," alisema Kamwe.

Alisema baada ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji kesho, kikosi kitaondoka Jumatano kuelekeza Zanzibar tayari kwa mchezo dhidi ya Al Ahly, Jumamosi ijayo.